Shirikisho la soka nchini TFF limemuandikia barua Rais wa Jamuhuri ya Muungano Wa Tanzania John Pombe Joseph Magufuli na kumuomba kuwa mgeni rasmi katika mchezo wa mzunguuko wa 29 wa ligi kuu ya soka Tanzania bara, kati ya mabingwa wa ligi hiyo Wekundu Wa Msimbazi Simba dhidi ya Kagera Sugar utakaochezwa uwanja wa Taifa, Dar es salaam, mwishoni mwa juma hili.
Rais wa TFF Wallace Karia amesema ombi hilo wamelifikisha kwa Rais Magufuli kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa Na Michezo ambayo inaongozwa na Harrison Mwakyembe, na wanaamini watapata majibu mazuri kwa Rais kufika uwanjani siku hiyo.
Karia ameeleza kuwa Rais Magufuli atapata wasaa wa kukabidhi kombe la 19 mabingwa wapya wa Ligi Kuu msimu huu wa 2017/18 ambalo wamelipata wakiwa hawajapoteza mchezo wowote msimu huu.
Mbali na Simba kukabidhiwa taji hilo katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, Magufuli atawakabidhi pia vijana wa Serengeti Boys Kombe la CEFACA chini ya miaka 17 walilolitwaa nchini Burundi baada ya kuifunga Somalia kwa mabao 2-0 kwenye mechi ya fainali iliyopigwa Uwanja wa Ngozi, jijini Bujumbura.
Sherehe za Simba na Serengeti Boys zitaanza majira ya saa 8 mchana huku viiingilio vya mchezo huo (Simba SC vs Kagera Sugar) vikiwa ni 15,000 kwa VIP A, 7000 kwa VIP B na C pia 3000 kwa sehemu ya mzunguko.