Rais wa awamu ya tatu wa Jamhuri ya Zimbabwe, Emerson Mnangagwa anatarajiwa kufika nchini Tanzania Juni 28, 2018 kwa ajili ya ziara ya kikazi ya siku mbili kuanzia Juni 28, 2018 hadi Juni 29, 2018.
Mnangagwa atapokelewa katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere International Airport Terminal I na mwenyeji wake hapa nchini Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli muda wa saa 5.00 asubuhi.
Ikumbukwe kuwa hii itakuwa ni ziara ya kwanza kwa Rais Mnangagwa kufika Tanzania kama Rais tokea aingie madarakani mwishoni mwa mwezi Novemba, 2017.
Ujio huu wa Rais Mnangagwa hapa nchini una lengo kuu la kuendelea kudumisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo baina ya nchi yetu na nchi ya Zimbabwe tangia wakati wa kupigania Uhuru wa Taifa hili la Kusini mwa Afrika.
Mnangagwa anatarajiwa kuondoka hapa nchini Juni 29, 2018 saa 8.00 mchana na atasindikizwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli.
Kufuatia ugeni huo, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema kuwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kwa niaba ya wananchi wote wa Tanzania wanawakaribisha wageni hao na wajisikie kuwa wako nyumbani muda wote watakapokuwa hapa jijini.