Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, ameishitaki kamati ya Bunge inayochunguza mashambulizi ya Januari 6 dhidi ya jengo la Bunge, akijaribu kuzuia kuitwa kwenye kamati hiyo ili kutoa ushahidi.
Kupitia wakili wake David Warrington, Trump amehoji iwapo marais wa zamani wamewahi kujitolea kwa hiari yao kutowa ushahidi ama nyaraka kwa maombi ya bunge, na ni kwanini hakuna rais aliyepo madarakani ama wa zamani aliyewahi kulazimishwa kufanya hivyo.
Alisema, “Trump ameshirikiana na kamati ya bunge kwa nia njema katika jitihada za kumaliza wasiwasi uliopo baina ya utawala na mtengano wa madaraka, lakini jopo linasisitiza kutumia njia ya kisiasa, na hivyo kumfanya Trump asiwe na jinsi ila kufika mahakama, kwenye mzozo huu baina ya utawala na wa bunge.”
Mashitaka hayo, yanaweka ugumu wa uwezekano wa Trump kulazimika kutoa ushahidi kwani kamati itavunjwa mwishoni mwa kipindi cha Bunge kinachokamilika Januari, 2023 na ilipiga kura kutaka Trump aitwe bungeni wakati wa kikao cha mwisho kilichotangazwa moja kwa moja kwa njia ya televisheni kabla ya chaguzi za katikati ya muhula.