Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amelitaka Shirikisho la Soka nchini humo kuhakikisha linaongeza bajeti ya chakula cha mlo kamili kwa ajili ya wachezaji wa timu hiyo ili kuwaongezea nguvu ya kupiga mashuti.
Akizungumza Jumanne wiki hii baada ya kufungua rasmi maadhimisho ya kumbukumbu ya Uhuru wa nchi hiyo, Museveni alisema kuwa ametoa maagizo hayo kwani aligundua kuwa mashuti waliyopiga nchini Gabon hayakuwa na nguvu za kutosha.
Hivyo, alilitaka shirikisho hilo kuhakikisha kuwa hali hiyo inatafutiwa ufumbuzi kabla ya mchezo dhidi Lesotho.
“Natumaini mameneja wanaweza kufanya kitu, kuboresha mlo wa wachezaji pamoja na mafunzo zaidi kuhakikisha kuwa wanakuwa na nguvu zaidi, kama alivyokuwa marehemu David Otii,” alisema Museveni.
Uganda Cranes wako katika nafasi nzuri kwenye mashindano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la mataifa huru nchini mwaka 2019, wakiongoza kwa alama 4 katika kundi L. Taifa Stars (Tanzania) na Cape Verde wanaunda pia kundi hilo.
Katika hatua ya kuwaongezea morali wachezaji, Museveni ameahidi kutoa ndege ya kuwasafirisha wachezaji hao kwenda Lesotho pamoja na kumpa kila mmoja fedha kama shukurani kwa kazi nzuri.