Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amewashukia baadhi ya viongozi wa dini kwa hatua zao za kukosoa mwenendo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Akizungumza katika hotuba yake ya mwisho wa mwaka 2017, Museveni ametoa kauli hiyo kufuatia hatua za baadhi ya viongozi wa dini kujitokeza na kupinga hatua ya Bunge la nchi hiyo kupitisha miswaada iliyowasilishwa na Serikali ya kuondoa ukomo wa umri wa kugombea nafasi ya urais pamoja na kuongeza muhula wa kuongoza kutoka miaka mitano hadi saba.

Rais Museveni amesema kuwa viongozi hao wa dini ni wasaliti kama kuhani mkuu aliyemsaliti Yesu kwani walipaswa kujikita katika kuzungumzia namna bora ya kuupata uhuru halisi wa Afrika na sio kuungana na harakati za mataifa ya Magharibi dhidi ya nchi hizo.

“Badala ya kufanya kazi kwa ajili ya uhuru wa Afrika, kila wakati wamekuwa wakiungana na mataifa ya nje kuyahamasisha yaingilie mambo yetu ya ndani,” alisema Rais Museveni.

“Hii tuchukulie kama hawana nia ovu dhidi ya nchi hii. Hii ingekuwa mbaya zaidi na ingewafanya wafanane na Kuhani Mkuu, Kayafa ambaye alimsaliti Yesu na kuandaa tukio la kumuua,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, alitumia vifungu vya Biblia kuwapa neno la shukurani wabunge walioshiriki kupitisha miswaada husika.

Alitumia kitabu cha Mathayo 5 : 11, “Mmebarikiwa ninyi wakati watu watakapowatukana na kuwatesa na kuwasingizia maovu kwa ajili yangu. 12 Shangilieni na kufurahi, kwa maana zawadi yenu huko mbinguni ni kubwa; kwa kuwa ndivyo walivyowatesa manabii waliowatangulia ninyi.”

Picha: Zawadi ya Papii Kocha kwa Rais JPM
Kisa cha raia wa kijerumani kuuawa kwa kisu Zanzibar