Rais Yoweri Museveni wa Uganda na Paul Kagame wa Rwanda wamesaini makubaliano ya amani katika mji mkuu wa Angola, Luanda kumaliza uhasama uliopo kati ya mataifa hayo jirani.

Wamefikia makubaliano hayo katika mkutano wa pili unaofanyika Luanda nchini Angola mbele ya marais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Angola na rais wa Congo Brazaville waliokuwa wapatanishi katika mgogoro huo.

Joto la kisiasa limekuwepo tangu mwanzoni mwa mwaka huu na limeathiri maisha ya watu, kijamii na kiuchumi katika mataifa hayo jirani.

Maafisa nchini Rwanda wameituhumu Uganda kwa kuwafunga na kuwatesa kinyume cha sheria raia wake nchini Uganda, wakati Uganda nayo ikiituhumu Rwanda kutekeleza ujasusi katika ardhi yake.

Katika hotuba yake aliyoitoa machi mwaka huu kwenye mkutano wa kitaifa, Rais wa Rwanda, Paul Kagame alisema kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na nchi ya Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita ambapo amesema kuwa nchi ya Uganda ilitaka kuangusha utawala wake.

Rais Kagame amesema kuwa mgogoro huo umeshika kasi hivi karibuni kufuatia wananchi wa Rwanda wanaoingia nchini Uganda au kufanya kazi nchini humo kushikwa na kuzuiliwa sehemu ambazo hazijulikani na kufanyiwa vitendo vya mateso huku akishutumu utawala wa Uganda kutoa nafasi ya ushirikiano kwa kundi la Rwanda National Congress linaloongozwa na mkuu wa zamani wa majeshi ya Rwanda jenerali Kayumba Nyamwasa.

”RNC wanafanya kazi kwa ushirikiano na vyombo vya usalama vya Uganda, kilicho wazi ni kwamba wanachokifanya ni kunyanyasa Wanyarwanda ambao hawataki kuungana nao huku wakiwasingizia kwamba wametumwa na utawala wa Kigali kuhujumu usalama wa Uganda, lakini haya yote yanaonyesha ushirikiano wa dhati uliopo baina ya serikali ya Uganda na kundi la RNC,”alisema Rais Kagame

Pia Uganda imekuwa ikiituhumu Rwanda kuwatuma majasusi na kufanya vitendo vya ujasusi kwenye ardhi yake, tuhuma ambazo Rwanda imezikanusha.

Hata hivyo, rais Kagame amesisitiza kuwa mara kadhaa mwenyewe aliwasilisha malalamiko hayo kwa mwenzake, Yoweri Museveni na kwamba hakuonyesha utashi wowote wa kuyatatua, ambapo kutokana na uhasama huo, Rwanda imeamua kufunga mpaka wake na Uganda wa Gatuna kwa usafiri wa bidhaa.

 

 

Video: Kinachoua majeruhi ajali ya Moro ni hiki, UN yaipongeza serikali matumizi ya rasilimali
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 22, 2019