Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi tayari yupo nchini Msumbiji, kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Mkutano huo wa siku moja wa dharura umeitishwa kuangazia masuala ya usalama na hatua za kukabiliana na vitendo vya ugaidi vinavyotokea kusini mwa Afrika, ambapo mbali na mwenyeji Msumbiji, mataifa mengine yatakayokuepo katika mkutano huo ni Afrika Kusini, Botswana, Zimbabwe, Malawi na Tanzania.

Awali rais wa Msumbiji Filipe Nyusi alisema ataitisha mkutano wa baraza la ulinzi na usalama lakini hakuweka wazi ni lini mkutano huo utafanyika.

Wanamgambo wa kiislamu walivamia mji wa Palma uliopo kaskazini mwa jimbo la Cabo Delgado Machi 24, na kuuwa watu kadhaa na mamia kulazimika kukimbia makazi yao huku wengine wakikimbilia Tanzania.

Kundi

Kundi la wanamgambo wa kiislamu (IS) ambao walidai kuhusika na shambulio hilo limelenga eneo hilo tangu Oktoba mwaka 2017, na hivi karibuni shambulio lao lililazimisha kampuni kubwa ya nishati ya Ufaransa kusitisha mipango yake ya uzalishaji wa gesi asilia katika eneo la Afungi Peninsula.

Rais Mwinyi aliondoka nchini jana Jumatano April 7, 2021 baada ya kumalizika kwa dua ya kumkumbuka Rais wa kwanza wa Zanzibar na mmoja wa waasisi wa Muungano wa Tanzania, Hayati Abeid Amani Karume iliyofanyika Kisiwandui mjini Unguja, Visiwani Zanzibar.

Young Africans yakataa kubebwa kimataifa
Hitimana: Vicent Barnabas ni tatizo Mtibwa Sugar