Sera ya mambo ya nje ya Diplomasia ya Uchumi kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ina haja ya kuimarishwa kwa manufaa ya pande zote za Muungano ili Zanzibar nayo ipate kunufaika vyema.
Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dtk. Hussein Mwinyi alipokutana na ujumbe maalumu wa Wizara ya Mambo ya Nje ulioongozwa na Waziri wa mambo ya nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula alipotembelea Ikulu visiwani Zanzibar.
Rais Dkt Mwinyi ameongeza kuwa uchumi wa Zanzibar kwenye mambo ya nje unategemea zaidi kazi zitakazofanywa na Mabalozi wanayoiwakilisha Tanzania nje ya nchi hasa ikizingatiwa kwamba Zanzibar ina bidhaa nyingi za kuuza nje ya nchi zikiwemo viungo na matunda.
Pamoja na hayo, Rais Dkt Mwinyi, amegusia suala la kutazamwa namna ya kuwapa hadhi raia wa mataifa mengine wenye asili ya Tanzania waishio nje maarufu kama Diaspora ili wapate hadhi maalumu ya kufanya baadhi ya masuala muhimu ikiwemo umiliki wa ardhi.
Aidha, Rais Mwinyi ameitaka Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuongeza juhudi za kuinadi sera ya Uchumi wa Buluu ambayo ni sera kuu ya kiuchumi na kipaumbele kikuu cha Serikali ya Awamu ya Nane anayoingoza.
Naye Waziri Mulamula na ujumbe wake, wamemshukuru Rais Mwinyi na kuahidi kufanyia kazi yale yote aliyowataka ikiwemo kuongeza wigo wa kuvutia wawekezaji wa nje na utalii visiwani Zanzibar pamoja na ushirikiano wa kimuungano kwenye masuala ya mambo ya nje.