Mshambuliaji wa Mabingwa wa Ufaransa Paris Saint-Germain Kylian Mbappé lazima asaini mkataba mpya ikiwa anataka kubakia katika klabu hiyo, kwani uongozi wa klabu hiyo hautakubali kumuacha aondoke bure mwishoni mwa msimu ujao 2023/24.

Kauli hiyo ya amri imetolewa na Rais wa klabu hiyo, Nasser Al-Khelaifi ambaye amekuwa akipendezwana uwepo wa Mbappe katika kikois cha Paris Saint-Germain.

Mbappé alituma barua kwa PSG mwezi uliopita ikisema kwamba hana nia ya kuongeza mkataba wake ambao unamalizika mwaka 2024.

Lakini baadaye alifafanua kwamba hakuiomba klabu hiyo ya Ufaransa imruhusu kuhamia kwa miamba ya Hispania, Real Madrid, ambayo siku za nyuma ilijaribu na kushindwa kumpata fowadi huyo aliyeshinda Kombe la Dunia mwaka 2018.

PSG wanakabiliwa na tatizo la kumpoteza Mbappé bure kama hatasaini mkataba mpya msimu huu wa joto na hivyo watakuwa wameingia hasara ya kushindwa kurejesha kitita cha euro milioni 180 walichotumia mwaka 2017 kumsajili kutoka AS Monaco.

“Msimamo wangu uko wazi sana. Sitaki kurudia kila mara; kama Kylian anataka kubaki anatakiwa kusaini mkataba mpya,” alisema Al-Khelaifi akiwaambia waandishi wa habari baada ya kumtambulisha Luis Enrique kama kocha mpya wa klabu hiyo.

“Hatutaki kumpoteza mchezaji bora zaidi duniani kwa uhamisho wa bila malipo hatuwezi kufanya hivyo. Hii ni klabu ya Ufaransa.

“Hataondoka bure. Ikiwa atabadilisha mawazo yake leo, sio kosa langu. Hatutaki kumpoteza mchezaji bora wa dunia bure, hilo liko wazi.”

Mbappé alimaliza kama mfungaji bora wa Ligue 1 katika misimu mitano iliyopita, na PSG watakuwa na nia ya kumbakisha, wakiwa tayari wamempoteza Lionel Messi kwa uhamisho wa bure.

Messi, mshindi wa Ballon d’Or mara saba, aliamua kutoongeza mkataba wake na kuhamia Inter Miami.

Ihefu FC yaachana na Kocha Simkoko
Tanzania Prisons kusajili sita 2023/24