Rais Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Kattanga, kuifumua Bohari ya Dawa (MSD), kuanzia Mkurungenzi Mkuu, Kitengo cha Ununuzi na idara nyingine.
Ameyasema hayo leo Marchi 30, 2022 wakati akipokea ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na ripoti ya Takukuru Chamwino, mjini Dodoma.
Rais Samia amesema kuwa ripoti ya CAG, Charles Kichere imebaini upungufu wa kiuendeshaji katika Bohari Kuu ya Dawa nchini (MSD) uliosababaisha kuwepo kwa uhaba mkubwa wa dawa nchini.
Akirejelea ripoti iliyowasilishwa na CAG, Rais Samia ametaka kufanyika kwa maboresho kuanzia ngazi ya chini hadi juu, ili kubaini kiini cha tatizo hilo.
“Bohari ya Dawa (MSD), inatakiwa kufanyiwa overhaul (maboresho) kama tulivyofanya kwa TANESCO, MSD walifikia hatua ya kupata tenda ya kuuza dawa SADC, lakini sasa hata humu ndani tu dawa hamna, kuzorota kwake kunatishia amani, japo SADC bado ina imani nayo” amesema Rais Samia.
“Naagiza overroll ifanyike kuanzia kwa Mkurugenzi Mkuu, Procurement Ukaguzi ufanyike kuanzia chini hadi juu kwa viongozi, kwa maana bado SADC wana imani na Tanzania.”
Kwa mujibu wa ripoti ya CAG, imeeleza kuwa MSD haikupeleka dawa licha ya kulipwa fedha za kusambaza dawa nchini, jambo ambalo limeifanya kushindwa kwa asilimia 66 kutimiza majukumu yake ya usambazaji wa vifaa tiba.
Ripoti hiyo imesema MSD inatakiwa kutimiza majukumu yake kwa asilimia 77, lakini hadi kufikia Juni 2021 ilitimiza asilimia 34 tu. na kuacha asilimia 66 zikiwa hazijatimizwa.