Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, ametaka ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma yenye urefu wa kilometa 112.3, ukamilike kwa wakati ili irahisishe shughuli za kimaendeleo katika jiji hilo.
Rais Samia amesema ujenzi wa barabara hiyo ya mzunguko haitawanufaisha wakazi wa Dodoma pekee bali na mikoa jirani.
“Tunafurahi kuweka jiwe la ujenzi wa barabara hii yenye umuhimu mkubwa sio tu kwa Dodoma lakini kwa Tanzania, mategemeno yetu ni kwamba mikoa ya jirani tunakwenda kuunganishwa nao wote kupitia barabara hii.”- amesema Rais Samia.
Rais Samia ameongeza kuwa si tu kwa mikoa jirani bali pia kwa nchi zilizo karibu na mikoa hiyo.
“Ndugu wananchi mradi huu, utakapokamilika utakuwa kichocheo Muhimu ya kukuza uzalishaji, barabara hii inakwenda kutupeleka kwenye masoko.”- ameongeza Rais Samia.
Rais Samia amesisitiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kupitia Wakala wa Barabara Nchini (TANROADS), kuhakikisha ujenzi unakamilika kama ilivyokusudiwa ili kutoa fursa ya kuleta maendeleo ya mmoja na Taifa kwa ujumla.