Afarah Suleiman, Babati – Manyara.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amehitimisha Kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 Mkoani Manyara hii leo Oktoba 14, 2023.
Mwenge huo, ukiwa Mkonani Manyara umetembelea na kuzindua miradi zaidi ya 1,400 yenye thamani ya Shilingi Trilioni 5.3 ambapo sherehe za kuhitimisha mbio hizo zimefanyika katika Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, uliopo katika mjini Babati.
Ndani ya mwaka 2023 umekimbizwa kwa siku 196 kwenye Mikoa 31 na Halmashauri 195 chini ya Vijana sita ambao wamekimbiza mwenge huo kwenye km 27,437 ambapo kati ya Miradi 1,424 iliyopitiwa, Miradi saba yenye thamani ya shilingi bilion 7.9 ilikataliwa kutokana na dosari mbalimbli.
Katika uhitimishaji huo, Rais Samia ametoa wito Kwa Vijana kuchangamkia fursa ya Kilimo Biashara na Kilimo cha umwagijiaji akilenga kupunguza tatizo la ajira huku Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango akihimiza jitihada za makusudi za utunzaji wa Mazingira ili kulinda na KUTUNZA mazingira Kwa vizazi vijavyo.
Akiwakilisha salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema zaidi ya Bilioni 535.7 zimetolewa na serikali Kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya Maji, Barabara, Elimu na Afya.
Mwenge huo wa uhuru mwaka 2024 utazinduliwa Mkoani Kilimanjaro na kilele chake pamoja na wiki ya Vijana kitafanyika Mkoani Mwanza.