Rais, Samia Suluhu Hassan ameanza ziara yake Mkoani Kigoma, ambapo kabla ya kuwasili Mkoani humo alifungua kituo cha Umeme cha Nyakanazi, na kisha baadaye kufungua Hospitali ya Wilaya ya Kakonko iliyopo katika kijiji cha Itumbiko ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yake.
Rais Samia pia alifungua mradi wa maji katika eneo la Kanyamfisi Kakonko Mjini, na kabla ya ufunguzi huo pia alipata wasaa wa kuzungumza na wananchi wa Ruwenze, Geita na muda mfupi amefungua barabara ya Kabingo – Nyakanazi Kakonko mijini na kuzungumza na wananchi.
Baadaye aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya Kibondo Mjini – Nduta yenye urefu wa kilomita 25.9 na atahitimisha siku yake kwa kuzungumza na wananchi katika uwanja wa Kibondo, Mkoani Kigoma.
Wakielezea hisia zao baada ya Rais huyo wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufanya ufunguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, baadhi ya Wananchi wamesema afya ndio mtaji wa kila mmoja wao na kwaamba bila afya hakuna matumaini, imani, maendeleo endelevu na ustawi katika jamii.