Kanisa la Good News Ministry limemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kutatua changamoto ya Raia wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi kupata fursa ya kuwekeza nchini na kuwawezesha kupata Uraia pacha.

Ombi hilo limetolewa leo Mei 12, 2021 na Askofu wa Kanisa hilo, Charles Gadi alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam, ambapo amesema kuwa Tanzania imekuwa ikiwakosa wawekezaji wazawa kutokana na sheria kandamizi zinazowanyima haki Watanzania waishio ugaibuni kumiliki mali na Ardhi Tanzania.

Askofu  Gadi amebainisha kuwa awamu za serikali zilizopita zilikuwa zinawaahidi watanzania kuja kuwekeza nyumbani lakini baadhi yao waliishia kunyang’anywa mali zao hali inayowapelekea Watanzania hao kushindwa kuja Tanzania kuwekeza.

Aidha ameongeza kuwa serikali ya Tanzania inatakiwa kuangalia upya sheria na kanuni zake za ardhi ili kuweza kuwapa fursa Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine kuweza kumiliki ardhi na kufanya uwekezaji nchini mwao.

Askofu huyo amemuomba Rais Samia kushughulikia suala la kibiashara baina ya nchi ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ili kumaliza sintofahamu iliyopo inayopelekea Wakongo kutotumia bandari ya Dar es salaam.

Amemshauri  Rais Samia kufanya ziara nchini Kongo, ili kukutana na wafanyabiashara ambao awali walikuwa wakipitisha mizigo yao katika bandari ya Tanzania na kuweza kujua tatizo lililowapelekea kusitisha kutumia bandari hiyo kwani hilo linaifanya Tanzania kukosa mapato ya Mizigo.

Watatu washikiliwa kwa mauaji
Kampuni yatangaza nafasi za kazi za kulala