Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameamua kuongeza fedha za motisha kwa timu za Simba na Yanga kutoka shilingi Milioni 5 hadi Shilingi Milioni 10 endapo timu hizo zitafuzu kucheza nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Simba inacheza mchezo wa marudiano leo dhidi ya Wydad Casablanca nchini Morocco wakati Yanga itacheza mchezo wa marudiano siku ya Jumapili (keshokutwa) dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Simba inacheza mchezo wa marudiano ikiwa na mtaji wa ushindi wa 1-0 ilioupata katika mchezo wa kwanza wa robo fainali uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam wakati Yanga itacheza mchezo wa marudiano ikiwa na mtaji wa ushindi wa 2-0 ilioupata ugenini huko nchini Nigeria.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anazitakia kila la kheri Simba na Yanga na amewataka wachezaji kujituma uwanjani na kutumia maarifa yao yote kuhakikisha wanashinda michezo ya kukamilisha robo fainali ili wafanikiwe kuingia nusu fainali ambapo kila goli litakuwa shilingi Milioni 10.
Aidha, Msigwa amesema magoli yatakayolipiwa shilingi Milioni 10 ni yale yatakayofungwa katika dakika 90 za mchezo au dakika 120 na sio magoli ya penati.