Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri pamoja na kufanya uteuzi wa wabunge watatu.

Akitangaza mabadiliko ya baraza hilo leo Jumatano Machi 31, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, katika hafla ya kumuapisha Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango,

Ambapo, Rais Samia amesema wabunge aliowateua ni Bashiru Ali Kakurwa, Balozi Liberata Mulamula na Balozi Mbarouk Nasoro Mbarouk.

“Kuondoka kwa Dk Mpango kumeacha nafasi ndani ya Wizara ya Fedha na tupo kwenye Bunge la Bajeti ambalo Waziri wa Fedha ni muhimu sana, sasa nikasema nisifanye kazi kidogo kidogo, hii imenifanya nilitazame baraza lote la mawaziri hivyo nimefanya mabadiliko madogo, wanasema zege hailali ni hapa hapa,” amesema Rais Samia

Katika uteuzi wake Rais Samia amemteua Ummy Mwalimu kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tamisemi huku manaibu Waziri wakibaki kuwa walewale, Festo Lugange na David Silinde.

Ofisi ya Makamu wa Rais, Waziri anakuwa Suleiman Jafo, Naibu waziri ni Hamad Chande, ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji imeondolewa kwenye ofisi ya Rais na kupelekwa chini ya Waziri Mkuu, Waziri akiwa ni Geofrey Mwambe huku Naibu Waziri akiwa ni William Ole Nasha.

Wizara ya Fedha na Mipango, Waziri ni Mwigilu Nchemba na Naibu Waziri ni Hamadi Masauni na Wizara ya Katiba na Sheria, Waziri ni Palamagamba Kabudi na Naibu Waziri ni Jose Mizengo Pinda.

Huku Wizara ya Mambo ya Nje, Waziri ni Balozi Leberata Mulamula na Naibu Waziri ni Mbarouk Nasoro Mbarouk na Wizara ya Biashara na Viawanda, Waziri ni Profesa Kitila Mkumbo, Naibu Waziri ni Exaudi Kigae.

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Waziri ni Innocent Bashungwa huku Naibu Waziri akiwa ni Pauline Gekul.

Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Waziri ni Dorothy Gwajima, Naibu Waziri ni Godwin Molel ambapo Mwanaidi Hamis amepeleka katika wizara hiyo na atashughulikia masuala ya maendeleo ya jamii na wanawake.

Kwa upande wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Waziri anabaki kuwa Mashimba Ndaki na Naibu Waziri ni Abdalah Ulega.

Rais ameeleza kuwa wizara nyingine zinabaki kama zilivyokuwa.

Dkt. Bashiru na wenzake wala kiapo Bungeni
Balozi Kattanga ateuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi