Umoja wa Machifu Tanzania (UMT) umempa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan jina la kichifu la ‘Hangaya’ lenye maana ya nyota inayong’ara
Rais Samia amesema kuwa anamuomba Mungu amjalie Ili aendane na maana ya jina hilo, huku akiwashukuru machief hao kwa heshima hiyo ya kumpatia jina lakini pia amewashukuru kwa kuendelea kumtia moyo katika kuliongoza Taifa.
“Katika Risala iliyosomwa nimesikia leo nimeitwa jina jingine na jina hilo ni ‘HANGAYA’, maana yake ni Nyota inayong’ara nawashukuru sana Umoja wa Machifu na Watemi kwa kunipa jina hili zuri sana, Namuomba Mungu niendane na jina mlilonipa HANGAYA, ‘Nyota Inayong’ara’, ning’are kweli kama nyota na sio ning’are mimi tu, niing’arishe nchi yangu. Namuomba Mungu anisaidie hilo,” Amesema Rais Samia.
Aidha Rais Samia amesema kuwa utamaduni ni moja ya mambo muhimu katika kulitambulisha taifa akitolea mfano lugha ya kiswahili kwa upande wa Tanzania ni moja ya utamaduni wa kulitambulisha Taifa, huku akisoma nukuu ya Baba wa taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere kuhusian na masuala ya Utamaduni.
“Baba wa Taifa Mwl Julius kambarage Nyerere aliwahi kusema utamaduni ni kiini ama roho ya taifa lolote, taifa lisilo na utamaduni ni sawa na mkusanyiko wa watu usio na roho,” Amesema Rais Samia.
Ameongeza kuwa Utamaduni unasaidia kueleza historia ya mila pamoja na desturi za jamii ya mataifa husika, pia Utamaduni unasaaidia kulinda au kutunza, kuendeleza na kurithisha maadili kutoka kizazi kimoja hadi kizazi kingine.
Sambamba na hayo yote ameupongeza umoja huo kwa kuandaa Tamasha hilo la utamaduni huku akiwaasa kuliendeleza tamasha hilo Mkoa hadi Mkoa ambapo Rais Samia amesema ataandaa kombe la Hangaya.