Rais Samia Suluhu leo amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Kenyatta uliowasilishwa na Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi wa Kenya, Balozi Dkt. Amina Mohamed.
Pamoja na kupokea ujumbe huo Ikulu Dar es saalam, Rais Samia amefanya mazungumzo na Balozi Amina kuhusiana na dhamira ya Tanzania na Kenya kuendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano katika nyanja mbalimbali hususani kiuchumi na kijamii.
Rais Samia amemuhakikishia Rais Kenyatta kuwa Serikali anayoiongoza ipo tayari kuendeleza mambo mazuri yote yaliyokuwa yakifanywa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli na kutatua changamoto kati ya Tanzania na Kenya kwa kuwa nchi hizi za Jumuiya ya Afrika Mashariki ni ndugu, majirani na marafiki wa kihistoria.
Rais Samia amewataka Mawaziri na Wataalamu wa Tanzania na Kenya wanaounda Kamati ya Ushirikiano wa Pamoja (JPC) ambao hawajakutana tangu mwaka 2016 kukutana mara moja ili kufanyia kazi masuala mbalimbali ya kuimarisha uhusiano.
Kupitia ujumbe huo, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemwalika Rais Samia kufanya ziara rasmi nchini Kenya ili kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano baina ya Tanzania na Kenya.
Rais Kenyatta amemuhakikishia Rais Samia kuwa Kenya ipo tayari wakati wote kushirikiana na Tanzania kwa kuendeleza na kukuza zaidi ushirikiano kati ya nchi hizi mbili.
Rais Samia amepokea mwaliko huo kupitia kwa Balozi Amina, ambaye ni Mjumbe Maalumu wa Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta akiwa ameongozana na Balozi wa Kenya nchini, Dan Kazungu.