Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameridhia uamuzi wa Serikali ya Indonesia wa kufufua shughuli za Kituo cha Mafunzo ya Kilimo kwa Wakulima Vijijini – FARTC, kilichopo Mkindo mkoani Morogoro.

Rais Samia amesema hayo hii leo Agosti 22, 2023 akiwa na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Indonesia Joko Widodo aliyepo nchini kwa ziara ya kiserikali ya siku mbili wakati wakizungumza na vyombo vya habari.

Amesema, kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 1996 na Serikali ya Indonesia kimechangia kwa kiasi kikubwa kuelimisha wakulima na kutoa mafunzo kwa wataalam wa kilimo.

Aidha, Rais Samia pia amesema Tanzania na Indonesia zimekubaliana kukuza biashara na uwekezaji kwa kuzileta pamoja sekta za umma na binafsi ili kuimarisha ushirikiano katika viwanda, kilimo, nishati, madini, mafuta na gesi, uvuvi na utalii.

Majadiliano yao yamebainisha nia ya Tanzania kupata uzoefu wa uzalishaji mafuta kutoka kwa Indonesia ambaye ni mzalishaji mkubwa zaidi wa mafuta ya mawese duniani, ambapo Serikali ya Tanzania imejidhatiti kuongeza uzalishaji wa mafuta ya kula, ili iache kutumia fedha zake za kigeni kuagiza mafuta nje.

Nchi hizo mbili zimetiliana saini hati 7 za Makubaliano (MoUs) ikiwemo sekta za ulinzi, nishati, kilimo, mifugo, uvuvi na uchumi wa buluu, madini, na pia misamaha ya viza kwa wamiliki wa hati za kusafiria za kidiplomasia na za huduma.

Viongozi wa Mikoa shughulikieni kero za Wananchi - Dkt. Mpango
Kwanini Kemikimba kaondolewa kazini?