Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ametajwa katika orodha ya watu mashuhuri wenye ushawishi mkubwa zaidi duniani kwa mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Jarida la TIME, Rais Samia ametajwa kutokana na sababu zilizochagizwa na uongozi wake wa kuvutia kuanzia mwanzo alipoingia madarakani Machi 2021.
Orodha hiyo imewataja viongozi wa mataifa mbalimbali akiwamo Rais wa Urusi Vladimir Putin, Rais wa Marekani Joe Biden, Rais wa China Xi Jingoing, pamoja na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy.
TIME linakuwa la pili kumtaja Rais Samia kwenye orodha ya hadhi ya juu, baada ya kutajwa na Jarida la Forbes, Disemba 2021 kama mmoja wa wanawake 100 wenye nguvu zaidi duniani.
Katika orodha hiyo ya TIME, wameandika maelezo machache yenye kumuelezea Rais Samia na vigezo vilivyochangia jina lake kuwepo katika orodha hiyo.
“Rais Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani Machi 2022, na uongozi wake umekuwa wa kipekee. Kwa mwaka moja tu ameshafanya mabadiliko makubwa kwa Tanzania. Amefungua milango ya mazungumzo na vyama vya upinzani, hatua zimechukuliwa kujenga upya imani kwenye mfumo wa kidemokrasia, juhudi zimechukuliwa kuimarisha uhuru wa vyombo vya habari, na wanawake na watoto wamepata mfano mpya wa kuigwa,” Times 100 imeandika.
TIME imekumbusha kuhusu hotuba ya Rais Samia ya Septemba 2021 kwenye Bunge la Umoja wa Mataifa akiwa ni kiongozi wa tano mwanamke kutoka Afrika kuwahi kulihutubia Bunge hilo.
Aliyekuwa Rais wa kwanza wa Liberia na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, Ellen Sirleaf aliliambia Jarida hilo jinsi alivyoipokea hotuba ya Rais Samia kwenye Bunge la Umoja wa Mataifa.
“Alipokuwa anazungumza maneno yenye nguvu, sikuwa na la kufanya zaidi ya kufikiria jinsi ambavyo mabega ya viongozi wanawake yana nguvu na jinsi wanavyoweza kuleta mabadiliko,” alisema Sirleaf.