Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameipongeza timu ya Young Africans kwa kufanikiwa kutinga Fainali ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kwa kuifunga Marumo Gallants ya Afrika Kusini.
Young Africans ilikamilisha mpango wa kwenda Fainali ya Michuano hiyo jana Jumatano (Mei 17) katika mchezo wa Mkondo wa Pili, huku ikipata ushindi wa 2-1 ambao unaifanya klabu hiyo ya jijini Dar es salaam kuibuka na ushindi wa jumla wa 4-1.
Rais Samia ametoa pongezi hizo leo Alhamis (Mei 18) Mchana alipozunguza katika hafla ya Azam Media jijini Dar es salaam, huku akitangaza Motisha ya Shilingi Milioni 20 kwa kila bao litakalofungwa na Young Africans katika hatua ya Fainali.
“Kwa upande wa serikali tutatoa Tsh. 20 milioni kwa kila goli pamoja na kutoa ndege ya kwenda, itawasubiri kisha itawarudisha”
“Pesa hizo zitatolewa iwapo Yanga itapata ushindi katika mchezo husika. Hakutakuwa na Pesa itakayotolewa iwapo Yanga atafungwa au kutoka sare.
Katika hatua nyingine Rais Samia ametangaza usafiri wa ndege kwa Young Africans itakapoelekea nchini Algeria kwa ajili ya mchezo wa Mkondo wa Pili wa Fainali dhidi ya USM Algiers iliyofanikiwa kuitoa ASEC Mimosas ya Ivory Coast kwa ushindi wa jumla wa 2-0.
“Serikali itatoa ndege kwa Yanga SC kuwapeleka katika mchezo wa fainali. Ndege hiyo itabeba wachezaji na mashabiki”
“Naomba sana wale viongozi wa TFF muwape moyo kama serikali tunavyofanya. Muwasemee vizuri ili wakapate ushindi” amesema Rais Samia
Mchezo wa Fainali Mkondo wa kwanza umepangwa kupigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam Mei 28, huku mchezo wa Mkondo wa Pili ikipangwa kupigwa Juni 04 mjini Algiers.