Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo matatu kwa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) katika kuelekea kuadhimisha miaka 60 ya Uhuru Desemba 9 mwaka huu.

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Octoba 23, 2021 katika maadhimisho ya kilele cha wiki ya UWT kitaifa yaliyofanyika wilayani Rufiji mkoani Pwani

Maagizo hayo ni pamoja na kutoa taarifa ya hali ya kiuchumi kwa Wanawake nchini, hali ya kisiasa kwa wanawake nchini pamoja na taarifa ya namna ambavyo Wanawake wamekombolewa kifikra nchini.

Ameitaka UWT kukaa na Taasisi ya ULINGO na kuandaa mkutano mkubwa kabla ya maadhimisho ya Sikukuu ya Uhuru na kueleza ni kwa kiasi gani wamefanikiwa kumkomboa Mwanamke kifikra, kiuchumi na kisiasa tokea Uhuru.

” UWT ilianzishwa kwa lengo la kuwakomboa Wanawake kifikra, kiuchumi na kisiasa, na hii ndio kauli mbiu ya maadhimisho yetu mwaka huu, hivyo niwatake UWT na ULINGO kuandaa mkutano mkubwa utakaogusia taarifa ya hali ya mwanamke katika nyanja hizo,” Amesema Rais Samia.

Akizungumzia Bibi Titi Mohamed, Rais Samia amesema Bibi Titi alikua ni mwanamke shupavu na shujaa ambaye alimsadia kwa kiasi kikubwa Baba wa Taifa Hayati Mwl Julius Kambarage Nyerere katika mapambano ya kudai Uhuru.

” Niwaombe Wanawake wote mlioko hapa tutoke tukiwa na moyo shupavu kama wa Bibi Titi, twendeni pamoja tukalitumikie kwa Taifa letu,” Amesema Rais Samia.

Rais Samia pia ameipongeza UWT kwa kufanikiwa kubadilisha mitazamo ya Wanawake na kuwa chanya, kufanya uwekezaji mkubwa katika sekta mbalimbali za kijasiriamali sambamba na elimu ambapo wamekua na Shule zao ambazo zimekua zikichangia ukuaji wa kiwango cha elimu nchini.

Pia ametoa wito kwa Wanawake wote kutoka na kauli mbiu moja yenye lengo la kupinga kwa nguvu tabia ya unyanyasaji na matukio ya ukatili wa kijinsia kwa Wanawake na Watoto nchini.

” Niwaombe wote kutoka na kauli moja ya kupinga tabia za ukatili kwa Wanawake na Watoto, ni ukweli kuwa wanawake tumekua tukichangia vitendo hivi kwa kutototoa taarifa kwenye vyombo husika au kuunga mkono vitendo hivyo tu kwa sababu aliyefanyiwa siyo Ndugu yako ama Mtoto wako,” Amesema Rais Samia.

Spika Ndugai ateta na Asasi za kiraia
Kigogo NIDA afutiwa mashtaka 10 na DPP