Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameelekeza Sheria za Habari ambazo zimekuwa zikilalamikiwa kuminya uhuru vya vyombo vya habari zirekebishwe.
Rais Samia ameyasema hayo leo Jumanne Mei 3 ,2022 wakati akiwahutubia Wadau wa Vyombo vya Habari kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari ikiongozwa na kauli mbiu ‘Uandishi wa habari na changamoto za kidigiti’
“Nimeelekeza Sheria zirekebishwe lakini kwa majadiliano pande zote na sit u kwamba sisi tunataka nini. Nimemwelekeza Waziri sheria za habari zirekebishwe kwa kushirikisha wadau wote”,amesema Rais Samia.
Rais Samia pia ameshauri waandishi wa habari kuwa Wazalendo kwa kuandika mambo mazuri za kutetea Bara la Afrika huku akiwataka waandishi wa habari kuzitangaza mila na desturi nzuri za Tanzania.
“Tunazo mila na desturi tunapaswa kuzilinda, na nyinyi waandishi wa habari mnatakiwa kuzilinda ili kuepuka mmomonyoko wa maadili katika jamii yetu. Baadhi ya watu wanapost picha chafu mtandaoni, wanajianika mtandaoni, wengine wanafanya hivyo kwa kututojua madhara ya kufanya hivyo. Wa kwenda kuzionesha changamoto za kidigitali.” ,amesema Rais Samia.
Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema Rais Samiaa amefanya mapinduzi makubwa katika tasnia ya habari kwa kipindi kifupi.
“Matumizi ya busara hayamaanishi kuwa sheria na kanuni zimefutwa, Sheria na Kanuni hizi hazijafutwa busara inatumika, tunatumia busara ili mambo yaende. Busara hii ni vizuri ikaheshimiwa. Msinitie majaribuni, naomba mnisaidie tupite kwenye kipindi cha mpito salama wakati tukipitia maboresho ya sheria hizi, tutahakikisha maoni ya kila mtu yanalindwa”,amesema Waziri Nnauye.