Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ametoa pole Watanzania, wanafamilia kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri wa Fedha na Utawala wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na Waziri Mstaafu wa Wizara tofauti kwenye Serikali ya awamu ya kwanza na pili, Al noor Kassum.
“Rais Mheshimiwa Samia amenituma niwape pole ndugu, familia na wote walioguswa na kifo cha Mzee Al noor Kassum. Mzee Kassum amefanya mambo makubwa sana kwenye nchi hii. Ametumikia Taifa kwa weledi, uaminifu na uadilifu mkubwa, Watanzania hatuwezi kumsahau,” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa .
Aidha Salamu hizo za pole zimetolewa leo Novemba 20, 2021 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipomuwakilisha Rais Samia katika kuaga mwili wa Marehemu Kassum kwenye viwanja vya Karimjee mkoani Dar es Salaam.
Hata hivyo Waziri Mkuu ametoa wito kwa watumishi wa umma kuyaendeleza yote mazuri aliyoyafanya wakati wa utumishi wake ili Taifa liendelee kushamiri kwa maendeleo na amani. “Tuliokuwepo kwenye madaraka tuendeleze utawala unaojali wananchi kama alivyokuwa akifanya marehemu.”
Pia ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kila mmoja kwa imani yake waendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu Mzee Al noor Kassum.
Naye Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema marehemu Mzee Kassum alimfundisha namna ya kufanyakazi na kuishi vizuri kati ya Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Waziri. Alimpokea wizarani alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Nishati, Maji na Madini wakati huo Mzee Kassum akiwa Waziri wa Wizara hiyo.