Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa Mwanamke wa kwanza kutunikiwa Shahada ya Heshima ya Udaktari wa Falsafa (Honoris Causa), na Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha Nchini India na kuitoa shahada hiyo kwa watoto hususan wa kike wanaoishi katika mazingira magumu nchini.
Akiipokea Shahada hiyo, ambayo ni ya kwanza kwake kutoka ugenini, Rais Samia amesema anakishukuru Chuo hicho kwa kumpa heshima hiyo ambayo ni kubwa na kwamba anaitoa kwa watoto wa kike wa Tanzania wanaoishi katika mazingira magumu na amewaka kutokukata tamaa huku akiisihi jamii kushirikiana kuwawezesha watoto hao kufikia ndoto zao.
Ameeleza kuwa, kitendo cha kuitoa tuzo hiyo kwa watoto hao kutokana na mazingira halisi aliyopitia tangu akiwa shule ya msingi hadi kufikia nafasi aliyonayo nayo sasa, huku akiwashukuru watu mbalimbali wakiwemo wazazi wake, familia, Chama cha Mapinduzi – CCM na wananchi wa Tanzania kwa mchango wao uliomwezesha kufikia hatua hiyo muhimu katika maisha.
“Shahada hii inanikumbusha mbali nikiwa mtoto mdogo nikienda shule katika kijiji nilichozaliwa cha Kizimkazi huko Unguja, Zanzibar, huku mama yangu akiwa ni mama wa nyumbani na baba mwalimu. Nawashukuru kwa kunipatia muda ulioniwezesha kufikia ndoto zangu za elimu, siasa na hatimaye kufikia nafasi niliyo nayo sasa,” amesema Rais Dkt. Samia.
Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Santishree Dhulipudi Pandit amesema wametunuku Rais Samia Shahada hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na India, Diplomasia ya Uchumi, mchango wake katika maisha ya kila siku ya wananchi wa Tanzania na mafanikio yake kikanda na kimataifa.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Dkt. Subrahmanyam Jaishankar ameielezea Shahada hiyo kama alama ya kuimarika kwa ushirikiano kati ya Tanzania na India.