Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema amefanya mabadiliko ya muundo wa Wizara mbili zilizohusiana na maswala ya habari ambapo ameitoa idara ya Habari kutoka Habari Utamaduni Sanaa na michezo na kwenda Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Rais Samia amefanya mabadiliko hayo ili kutimiza ndoto ya muda mrefu ya watu wa sekta ya habari na kuifanya Wizara ya Habari Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kutimia.
Ameyasema hayo leo Septemba 13, 2021 wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali walioteuliwa, huku akielezea sababu zilizomfanya kufanya mabadiliko hayo ikiwa ni pamoja na kutoa msukumo mkubwa kwa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwasababu ilikuwa inamezwa kwa kiasi kikubwa na idara ya Habari.
“Nimeona niiiachie ionekane kwa uwazi zaidi kwasababu Sanaa, Utamaduni ni Michezo ni ajira kwa vijana wetu wengi sana lakini pia ni utalii,” Amesema Rais Samia.
Hata hivyo Rais Samia amesema kuwa kwa kuipa nafasi Sanaa na Utamaduni itasaidia pia kukuza jina la Nchi.
Sambamba na hayo, Rais Samia amesema amevunja tafsiri mbaya ya muda mrefu kuwa Wizara nyeti huongozwa na mwanaume kwa kumteua Stegomena Tax kuwa waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga taifa.
“Kazi ya Waziri sio kupiga mitutu bali kuhakikisha kila jambo liko kwenye mstari wake na Kipindi cha SADC alikuwa anasimamia vema hivyo atakwenda kutusaidia,” Amesema Rais Samia.
Aidha Rais Samia amewaasa viongozi hao walioteuliwa kufanya kazi kwa bidii kwani anachotaka ni kuona matokeo kwa haraka na amewataka kufanya mabadiliko pale wanapodhani panahitaji mabadiliko.