Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka Vijana na Wakulima kujielekeza katika kilimo cha biashara, na kwamba utekelezaji wa ajira za Vijana katika sekta ya Kilimo tayari umeandaliwa mpango utakaohakikisha mapinduzi katika sekta hiyo yanafanikiwa.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo Agosti 8, 2022 katika kilele cha cha maadhimisho ya Sikukuu ya Wakulima (Nanenane), ambayo yamefanyika katika uwanja wa John Mwakangale Mkoani Mbeya na kudai kuwa hatua hiyo itaendana na utafutaji wa masoko katika nchi za nje.
“Vijana njooni katika Kilimo, huku kuna fursa nyingi na mkumbuke tayari Waziri Mkuu amezindua jambo katika masuala ya Kilimo jikiteni kwenye sekta hii kuna mipango mizuri na fursa za kutosha na hela ipo,” amesema Rais Samia.
Amesema, wakati serikali inatenga fedha za ruzuku kwa wakulima, pia wanatakiwa kujitahidi kufanya kilimo cha biashara kwa kuuza mazao nje na kuanzisha mifuko ya maendeleo ya kilimo, utakaosadia kupata pesa za kukabiliana na uhaba wa pembejeo katika kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Rais Samia ameongeza kuwa, “Serikali imefuta tozo nyingi kwa wakulina na hivyo zile zilizopo mnapaswa kulizipa kama ilivyokusudiwa, lengo ni kuleta mapinduzi chanya katika kilimo nchini na kuinua uchumi wa Taifa.”
Kuhusu tatizo la kutegemea viwanda vya mbolea kutoka nje, Rais samia amesema tayari mipango imeandaliwa na kuna viwanda ambavyo tayari vimejengwa huku vingine pia vikitarajia kuanza ujenzi wake katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha katika hatua nyingine, Rais ameilekeza Wizara ya Kilimo kuhakikisha mifuko ya mbolea inawekwa mifumo ya utambuzi na kampuni zilizosajiliwa, na kuhakikisha zinaweka mawakala wanaotambuliwa na Serikali ili kuondoa utata wa mbolea feki zinazosambazwa nchini.
Samia ameongeza kuwa, “Wizara ya Kilimo inatakiwa kuhakikisha inashiriki kikamilifu katika kuwasajili wakulima ambao watapatiwa ruzuku, na kuwataka wahusika kuhakikisha wanajisajili kwani baadaye vitatolewa vitambulisho vitakavyowasaidia kupata huduma.”
Akizungumzia miradi ya Kilimo, Rais Samia ameungana na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe kwa kusema miradi mingi ya kilimo inatakiwa iwanufaishe wakulima katika maeneo husika, na kuwataka maafisa ugani kuwa makini na matumizi ya rasilimali na vitendea kazi vya Serikali walivyopatiwa ili kuwahudumia wakulima.