Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF), kutowanyima baadhi ya watu fursa ya unufaika wa mfuko huo kwa kigezo cha vyeo walivyonavyo katika jamii.

Rais Samia ameyasema hayo hii leo Juni Mosi 2022 katika hafla ya kukabidhi magari 123 ambayo ni sehemu ya magari 241 yanayotarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya TASAF kwa Halmashauri zote nchini iliyofanyika viwanja vya Posta jijini Dar es salaam.

“Kuna jambo moja si zuri mnapoandikisha wanufaika kuna watu mnawatenga mtu anakubalika na ameaminiwa na jamii basi huyo hafai kwa kudhani kwamba anajiweza kimaisha hii si sawa,” amesema Rais Samia.

Amesema wapo viongozi wa vyama ikiwemo vya siasa ambao wameaminiwa na vyama vyao au jamii kutokana na utashi walionao hivyo nyadhifa zao zisiwazuie kufaidika na mpango wa TASAF ikiwa wana vigezo vyote vinavyoshahili kama mradi unavyoelekeza.

“Mnawakataa kwa kuwahukumu lakini wapo wanaoishi katika nyumba ambazo si rafiki kwa mazingira ya binadamu na uongozi wake haumfanyi kuwa tayari ameondokana na shida alizonazo,” amefafanua Rais.

Awali kabla ya kumkaribisha Rais Waziri wa Nchi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Jenista Mhagama amesema Rais Samia anaendelea kuweka historia kwa kujenga uchumi na amewathibitishia Watanzania jinsi anavyowajali kwa kuwapatia magari yatakayosaidia utekelezaji wa majukumu na kuwahudumia.

Amesema mradi wa huo wa TASAF awamu ya tatu sehemu ya pili utasaidia kuwafikia wahitaji katika vijiji, shehia na kaya zenye wakazi zaidi ya milioni sita na kufanya mpango huu wa maendeleo wa taifa kutekelezwa kwa ufanisi.

“Mheshimiwa Rais umewahakikishia Watanzania hasa masikini jinsi unavyowajali maana mradi huu umewafikia zaidi ya wakazi milioni sita na hii inatokana na juhudi zako za kuendelea kuinua uchumi wa nchi,” amesema Waziri Mhagama

Aidha amemuhakikishia Rais kuwa fedha zote za TASAF zitawafikia walengwa kwa wakati na kwamba watasimamia kwa uadilifu kazi zote zinazotekelezwa katika mradi huo ambao unatarajia kulea matokeo chanya.

Rasi Samia: TASAF muwainue wenye bidhaa zisizo na viwango
Majaliwa arudisha 'Kauli ya misitu ni Uhai'