Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewapongeza Wakenya kwa kufanya Uchaguzi Mkuu kwa amani.
Rais Samia, ametoa pongezi hizo kupitia ukurasa wake wa Twitter ambapo amesema, Tanzania itaendeleza undugu wa kihistoria na Kenya.
“Ninapenda kuwapongeza kwa dhati wananchi wa Kenya kwa kushiriki uchaguzi wao mkuu kwa amani na utulivu, ambapo matokeo yake ni Dkt William Ruto kutangazwa kuwa Rais mteule wa Kenya,” ameandika Rais Samia.
Ameendelea kuandika kuwa, “Tanzania itaendeleza undugu na ushirikiano wa Kihistoria na Kenya uliodumu miaka na miaka.”
Kenya, ilifanya Uchaguzi Mkuu Agosti 9, 2022 ambapo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ilimtangaza William Ruto kuwa Rais mteule wa nchi hiyo.
Ruto, alipata kura 7,176,141 ikiwa ni asilimia 50.49 ya kura zote, huku mpinzani wake, Raila Odinga akipata 6,942,930, sawa na asilimia 48.85 ya kura zilizopigwa.