Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi kuwapuuza watu walioanza kutoa kauli zinazoweza kupoteza amani iliyopo nchini.
Akizungumza na wananchi katika stendi ya mabasi ya Msamvu mjini Morogoro aliposimama kuwasalimu, alisema wapo baadhi ya watu wameanza chokochoko ambayo inalenga kusababisha vurugu.
“Kuna baadhi ya watu wameshaanza chokochoko naomba muwapuuze kwani hawawatakii wema, wanataka kuvunja amani ya nchi iliyopo kwa muda mrefu na kusababisha vurugu nchini,” alisema Rais Samia.
Kauli hiyo ya Rais imeleta tafakuri kwa wananchi. Hivi karibuni, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wameeleza hadharani kukaidi agizo la Rais Samia la kuendelea kuwa na subira na kutofanya mikutano ya hadhara kwa wasio wabunge na madiwani, wakidai kuwa wanajipanga kufanya mikutano hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari alipokuwa akihitimisha siku 100 za utawala wake, Rais Samia alisema anatambua umuhimu wa Katiba Mpya pamoja na ahadi yake ya kukutana na viongozi wa vyama vya siasa, lakini vyote vinapaswa kusubiri akamilishe hatua za awali za kupandisha uchumi.
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimeeleza kuwa kinajipanga kufanya mikutano ya aina hiyo nchi nzima na kuanzisha vuguvugu la kudai Katiba Mpya.
Katika hatua nyingine, Rais Samia aliwapongeza wakazi wa mkoa huo kwa kubarikiwa kuwa na miradi mikubwa ya kimkakati miwili ambayo ni Reli ya Kisasa (SGR) na Mradi wa Kufua Umeme wa Mwalimu Nyerere. Hivyo, aliwataka wananchi kuwa walinzi wa miradi hiyo.