Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassani hii leo Oktoba 17, 2022 amezima umeme wa jenereta na kuwasha umeme wa gridi ya Taifa na akiwasisitiza taka wananchi kutunza miundombinu iliyowekwa na kujibidiisha katika shughuli za kimaendeleo.
Rais Samia, baada ya kuwasha umeme huo wa gridi ya Taifa pia alizungumza na Wananchi katika ziara yake ya ya kikazi akiwa Wilayani Kasulu mkoani Kigoma na kusema umeme huo wa uhakika utasaidia kukuza shughuli za kiuchumi.
Amesema, “Pamoja na kwamba tumezima jenereta zilizokuwa zinatumika lakini tumeweka akiba majenereta haya, pamoja na kwamba yanatunzwa na shirika la umeme (Tanesco), lakini ni muhimu nasi kuyatunza yasiharibiwe na kituo hiki kibaki kama kilivyo.”
Rais Samia ameongeza kuwa, maendeleo yanayopatikana ni kwa ajili ya wananchi na kwamba serikali inajenga miundombinu ili kuwawezesha kufanya shughuli za kimaendeleo katika maeneo yao, hivyo ni jukumu la kila mmoja kujibidiisha.
“Mkoa wa Kigoma upo pembezoni mwa nchi ya Tanzania, na tumeleta umeme wa uhakika ili wawekezaji waweze kuja kwa wingi na kuwekeza katika mkoa huo, kama ni dhahabu basi ziweze kuchenjuliwa na wawekezaji kutoka nchi jirani.”
Kwa upande wake Waziri wa Nishati, January Makamba amesema umeme huo utasaidia kuondoa gharama nyingi za uendeshaji, zikiwemo za matengenezo na mafuta.
Amesema, “Umeme wa gridi kufika kigoma kuna manufaa makubwa sana ya kiuchumi, Mkoa wa Kigoma kwa vituo vyetu hivi vya kuzalisha umeme kwa majenereta ni megawati 14 lakini umeme uliokuja kwa gridi sasa hivi ni wa megawati 20.”
Hata hivyo, amesema kwa mwaka mafuta peke yake kwenye vituo vya kuzalisha umeme kwenye jenereta ni Shilingi 52 bilioni kwa mwaka, lakini mapato yanayopatikana ni Shilingi 14 bilioni.