Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amefungua Barabara ya Nyahua – Chaya Mkoani Tabora yenye urefu wa kilometa 85.4 na kusema Serikali haina mpango wa kuugawa mkoa huo licha ya kukiri kuwa baadhi ya Wilaya zake ni kubwa.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo Mei 17, 2022 na kudai kuwa kugawa maeneo kunaipa Serikali gharama na kwamba kwasasa suala lililopo ni kujenga uchumi kwanza kwani ulianguka kutokana na maradhi ya UVIKO 19.
“Wote mnajua uchumi wetu ulidondoka kutokana na maradhi ya Covid 19 tunajaribu kuujenga uje juu haraka kabla ya haya mnayohitaji maana kuna mahitaji mengi ya wananchi yanayotegemea fedha kutoka Serikalini,” amesisitiza Rais Samia.
Hata hivyo Rais amesema anaelewa kuwa baadhi ya Wilaya katika mkoa huo ni kubwa zikiwa na mzunguko mrefu kuyafikia makao makuu na zinahitaji kukatwa lakini akasisitiza kwa sasa haitowezekana.
“Mkoa wa Tabora ni mkubwa unahitaji kugawiwa mimi nasema endeleeni na mchakato wa kuangalia jinsi mnavyopenda ikatwe lakini hatutokata sasa tujenge uchumi kwanza” amesema katika hotuba yake.
Aidha amewataka wananchi kuhakikisha hawaharibu na wanaitunza miundombinu iliyopo kwani Serikali imetumia gharama kubwa katika ujenzi wake na kwamba historia inaonesha maeneo mengi yana vitendo vinavyohatarisha usalama wa barabara na madaraja.
“Vitendo hivi ni pamoja na uchimbaji mchanga kiholela, utupaji wa taka hovyo zaidi ya hapo wananchi wanadiriki hata kuiba alama za barabarani hii ni hatari na ni uhujumu wa uchumi wetu barabara lazima ziwe salama,” amesisitiza.
Kufuatia agizo hilo Rais Samia ameisisitiza Wizara ya Uchukuzi kupitia TANROADS kuendelee kusimamia viwango vya ubora na kasi ya utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa kuzingatia masharti ya mikataba.
Uzinduzi huo umefanyika Kijiji cha Tura kilichopo Wilaya ya Uyui Mkoani Tabora na umehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa huo Batilda Buriani, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa.
Wengine ni Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mhandisi Rogatus Mativila, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Kuwait (KFED) Waleed SH. Albahar, viongozi mbalimbali wa Serikali na Wananchi.