Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Juni 13, 2021 amezindua kiwanda cha kusafisha dhahabu cha Mwanza Precious Metal Refinery (MMPR) kilichojengwa kwa  Sh12.2 bilioni.

Hafla ya uzinduzi wa kiwanda hicho imehudhuriwa na wakazi wa Jiji la Mwanza, viongozi wa Serikali, kisiasa na kidini.

Kiwanda hicho cha kisasa cha kusafisha dhahabu (State-of-the-art Refinery), Mwanza Precious Metals Refinery (MPMR), kinamilikiwa kwa ubia kati ya Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) na wabia kutoka Dubai na Singapore.

“Ndugu zangu hivi punde nimezindua mtambo wa kusafisha dhahabu na nimeona mambo mazuri yaliyomo mle, na mtambo huu Pamoja na ujenzi wa kiwanda na ofisi mbili, kama mlivyosikia umegharimu dola milioni 5.2 au bilioni 12.2 kwa fedha za Kitanzania.” amesema Rais Samia

”Tumeambiwa mtambo huu ni mkubwa na wa kisasa ambapo uwezo wake ni kusafisha kilo 480 za dhahabu lakini zinaweza kuongezeka hadi kufikia kilo 960 kwa siku kwa kiwango cha juu kabisa cha kimataifa yaani dhahabu ya hapa itasafishwa kwa asilimia 99.9, karibu na asilimia 100”

“Wasiwasi wangu upo kwenye upatikanaji wa malighafi, kama kwa siku ni kilo 480, ingawa ndani ya mtambo huu kuna mashine ndogondogo zinazosafisha kilo 80 kwa siku nadhani ni kuendana na upatikanaji wa malighafi lakini nina wasiwasi mkubwa wa upatikanaji wa malighafi.”amesema Rais Samia

“Manufaa ya mtambo tumeyasikia, yapo mengi lakini nigusie machache. La kwanza ni kuongeza mapato ya serikali kupitia mrabaha au tozo za ukaguzi na ushuru wa huduma. Lakini pili utoaji wa ajira za moja kwa moja ambazo zinakisiwa ajira 120 zitakuwa za moja kwa moja na ajira 400” amesema Rais Samia

Naye Mtendaji mkuu wa kiwanda hicho, Anand Mohan ameishukuru Serikali kwa kufanikisha ujenzi wa kiwanda hicho huku akisema kitachangia kukuza uchumi wa Tanzania.

Ma- DC muwaambie wakulima watakavyonufaika - Majaliwa
TANZIA: Prof Mwesiga Baregu afariki dunia