Rais wa Jamhuri Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa fedha zilizokuwa zimepangwa kwa ajili ya maadhimisho ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka huu zigawanywe kwa pande mbili za Muungano.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango wakati akizungumza katika kongamano la miaka 57 ya Muungano linalofanyika jijini Dodoma.
Ameongeza, kila upande utaamua namna ya kutumia fedha hizo kwa shughuli za maendeleo.
Aidha, Dkt. Mpango amesema kuwa sababu ya mwaka huu kutofanyika sherehe za Muungano kama inavyokuwa miaka mingine, ni kutokana na kifo cha aliyekuwa Rais Dkt. John Magufuli.
“Mwaka huu kutokana na tukio la hivi karibuni ambapo nchi yetu iliondokewa na mmoja wa Mashujaa wake, Hayati Dkt. Magufuli, tuliamua badala ya Sherehe tuadhimishe Muungano kwa kuwa na Kongamano” amesema Dkt. Mpango.