Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anaondoka nchini leo kwenda Ghana ambapo atakuwa na ziara ya kikazi ya siku tatu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, akiwa nchini humo atashiriki mdahalo wa wakuu wa nchi utakaojadili fursa zilizomo na changamoto zinazozikabili nchi za Afrika ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi, kupanda kwa bei ya vyakula na matumizi ya nishati endelevu.
Aidha, Rais anatarajiwa kupokea Tuzo ya Mwaka 2022 ya Babacar Ndiaye aliyotunukiwa kutokana na mafanikio ya serikali ya awamu ya sita katika ujenzi wa miundombinu ya usafirishaji ambayo hutolewa kwa mkuu wa nchi iliyofanya vizuri.
Tuzo hiyo hutolewa kila mwaka katika mkutano wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambao kwa mwaka huu unafanyika Accra, Ghana.