Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inakwenda kutoa zawadi kwa wachezaji wote watakaoleta medali za mashindano ya madola yanayoanza nchini Uingereza hivi karibuni kama hamasa maalum kwa wachezaji.
Amesema kwa mara ya kwanza kabisa Serikali imeandaa zawadi dola 10000 kwa mshindi atakayerejea na medali ya dhahabu na
dola 7000 kwa mshindi wa medali ya fedha na mshindi atakayeshinda medali ya shaba atapata dola za kimarekani 5000.
Mhe, Mchengerwa ameyasema hayo leo Julai 20, 2022 kwenye hafla ya kuwaaga wachezaji wa Tanzania wanaokwenda kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola nchini Uingereza.
Katika hafla hiyo iliyofanyika Ukumbi wa Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam amewataka wachezaji kuweka uzalendo mbele na kuwataka kurudi na medali.
Amefafanua kuwa watambue kwamba dhamira ya Serikali kwa sasa ni kufanya mapinduzi makubwa ambapo amesisitiza kuwa watanzania wamechoka wanataka matokeo chanya katika mashindano haya.
Amesema Serikali imeacha kutoa fedha kwenye maeneo mengine kama afya, elimu na miundombinu na kuelekeza fedha kwenye michezo ili wachezaji waweze kufanya vizuri.
Ameongeza kuwa Serikali imegharimia timu hizo kuanzia Februari mwaka huu hivyo hakuna sababu ya timu hizo kutofanya vizuri.
Aidha, amesema wachezaji lazima kuzingatia nidhamu katika mashindano hayo.
Kwa upande mwingine ameitaka timu ya taifa ya Michezo wa kabaddi inayokwenda kwenye mashindano ya Afrika huko Misri kufanya vizuri ili kuwa timu ya tatu kuingia kwenye kombe la dunia.
Amewataka kwenda kuliheshimisha taifa kwa kutumia pia michezo hii kutangaza Royal Tour.
Aidha, ametumia hafla hiyo kuzindua kampeni ya kuwatumia wasanii na wanamichezo inayojulikana kama Sensabika ili wananchi wajitokeze kwenye sensa itakayofanyika Agosti 23, 2022.
Amesema kabla ya sensa kutakuwa na mchezo wa kukimbizana na ng’ombe.
Aidha amesema kutakuwa na tamasha la michezo, sanaa na utamaduni kwa ajili ya kuhamasisha sensa.