Miezi michache baada ya kueleza mpango wa kukutana na wapinzani, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesisitiza kuwa atatekeleza ahadi yake.

Akizungumza katika mahojiano maalum na BBC, Rais Samia amesema alikuwa anasubiri wapinzani wajiunde kwenye mabaraza yao ili aweze kuzungumza nao kwa mfumo huo.

Ameeleza kuwa kwa kipindi cha hivi karibuni, wapinzani wamefanya uchaguzi wa mabaraza yao ya kidemokrasia na sasa anaamini wako tayari katika mfumo ambao utamuwezesha kuzungumza nao na kuwaeleza muelekeo wa Serikali yake na siasa.

“Wamefanya uchaguzi wiki mbili zilizopita, ndio wamejiunda vizuri. Na kama wameshajiunda vizuri na kamati zao ndogondogo zimejiunda vizuri, basi tutatafuta tu siku tuitane tuzungumze vizuri,” amesema Rais Samia akisisiza kuwa itakuwa hivi karibuni muda ukipatikana.

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema kuwa ataendelea kuwashirikisha wapinzani kwenye Serikali yake, endapo ataona kuna mtendaji mzuri nje ya Chama Cha Mapinduzi atamuingiza kwenye Serikali yake ili ashiriki katika kujenga Taifa.

“Kwa sababu hata mimi nataka kuzungumza nao, niwaeleze muelekeo wangu kwamba uchaguzi umekwisha sasa twende tukajenge nchi. Na kwenye kujenga nchi mimi sichagui, nikimuona mpinzani amekaa vizuri ana muelekeo namuweka kwenye serikali yangu. Kwa sababu hakuna sehemu iliyosema baada ya uchaguzi, chama kilichojenga nchi peke yake ndio kitajenga nchi, hapana,” ameongeza.

KMKM uso kwa macho na mabingwa wa Uganda
Kifaa kingine kimeshushwa Biashara United Mara