Wananchi katika eneo la Mbezi makabe na Msumi jijini Dar es Salaam, wameiomba Serikali kumfuatilia Mkandarasi wa Ujenzi wa barabara yao ambaye anafikisha mwaka mmoja akiwa saiti akijenga kipande cha lami kutoka Aureke hadi Kanisani, ambacho hakijafika kilometa moja na kuhoji walipo watendaji na iwapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewasahau watu wa Msumi.
Wakizungumza katika mahojiano na Dar24 Media, Wananchi hao wameitaka pia Serikali kuwafikiria watu wa hali ya chini na kuwatambua kama nao ni binadamu na wanaishi, hivyo ijitahidi kuwatatulia kero zao za kijamii, ikiwemo kuwajengea miundombinu ya barabara kutokana na changamoto ya usafiri uharibifu wa vifaa vya magari unaowakabili.
Mmoja wa Wananchi hao, Samuel Nyamsange amesema, “hivi Serikali ipo wapi, watendaji TANROADS wapo wapi, inawezekanaje mkandarasi hamalizi kilometa moja ya lami zaidi ya mwaka na yupo saiti? na amekaa hapo hapo anachimba hapa anahamia pale na ukienda sasa hivi unamkuta hamalizagi huko Msumi sasa sio kuna barabara ni mahandaki.”
Amesema, wengi wa wanasiasa wamekuwa wakitumia lugha nzuri wakati wa kampeni lakini uhalisia wa vitendo ni mdogo na hali hiyo humuumiza mwananchi wa chini ambaye anachangia pato la taifa kupitia kodi anayokatwa bila kuona matunda yake kitu ambacho hakifai.
Kwa upande wake Juma Mbwana amesema, “na kibaya zaidi hizo STK (magari ya Serikali), zinapita humuhumu na hakuna hatua maana wao si wapo kwenye viyoyozi, shimo hawazisikii na ajabu sasa eti ukiwauliza jamani vipi nao eti wanashangaa halafu njia yenyewe wanajenga nyembamba ili baadaye waje tena kubomoa waiongeze mji unazidi kukua huu kwanini hawafanyi vitu kwa uhakika, hapa mtu akitamka neno baya kuna kosa?.”
Akijibu hoja hizo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Dar es Salaam, Haruon Senkuku amesema ujenzi wa barabara hiyo unakaribia kukamilika na kwamba matengenezo mengine yatafuata kila mwaka kwa urefu wa kilometa moja kwani huo ni mradi mdogo ukilinganisha na ule mkubwa kama wa BRT.