Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amewataka watanzania kutembea vifua mbele kwa mambo yaliyofanikiwa katika miaka 60 tangu uhuru wa Tanganyika hadi hii leo ukilinganisha na yaliyofanyika wakati wa ukoloni kabla ya Uhuru.
Rais Samia ameyasema hayo hii leo tarehe 08 Disemba akizungumza na watanzania kupitia vyombo vya habari katika hotuba maalumu aliyoitaja kama ujumbe wa miaka 60 ya uhuru kwa wananchi.
katika hotuba yake Rais Samia alianza kwa kuzungumzia uhuru ulivyopatikana na waasisi wa uhuru walivyopigana kuhakikisha wakoloni wanaachia nchi na kuwapatia nafasi waanziishi wa nchi kusimamia uchumi wao na wananchi wao.
“uhuru wa Tanganyika ulikua muhimu katika kuleta mapinduzi ya Zanzibar na kufanikisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar ambapo leo tunajivunia uhuru wetu na amani iliyotangulizwa na viongozi wetu” amesema Rais Samia.
Rais Samia ametaja umuhimu wa siku adhimu ya miaka 60 ya Tanzania bara pamoja na mafanikio yake kwa nchi ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kulinda uhuru wa nchi na amani ya Tanzania, Kuleta mshikamano kati ya wananchi na nchi nyingine, kuimarisha uchumi kutoka uchumi wa chini hadi uchumi wa kati, kuongeza upatikanaji na huduma za jamii kama usafiri wa barabara, reli, anga na majini, kujenga heshima ya nchi kimataifa na kuimarisha demokrasia ya wananchi.
“Nitoe pongezi kubwa kwa JWTZ, mmetulinda kwa ari na mali na ni fahari kubwa kuwa na jeshi ambalo linaitumikia nchi yake na hata kusaidia nchi za jirani katika kulinda amani yao, hii ni katika kulinda uhuru wa nchi na amani ya taifa zima kwa miaka yote 60 ya uhuru” amesema Rais Samia.
Katika faliniko la kuleta mshikamano kati ya wananchi na nchi nyingine Raisi Samia amezungumzia matumizi ya lugha ya kiswahili akisema wakati tunapata uhuru kiswahili hakikuzungumzwa na watu wote ila baada ya uhuru kilifundishwa mashuleni hivyo kufanya lugha hii kuwa lugha ya taifa na inatuweka pamoja, katika miaka 60 nchi imefanikiwa kushawishi jumuia ya ya kimataifa kuanza kutumia lugha hiyo katika mikutano yake na nchi washrikiaka kukifunzisha mashuleni.
“Wakati tunapata uhuru wakoloni walituachia kilomita chache za barabara na sasa mtandao wa barabara tulioujenga unaweza kutosha barabara za nchi nyingine. ATCL tuna jumla ya ndege 12 na malipo ya awali ya ndege nyingine 5, Majini jitihada zimefanyika kuanzia meli 6 kabla ya uhuru na sasa tuna meli 16 na vivuko 33 kwa mikoa yenye vivuko wakati Reli kwa sasa ni km 2707 ukilinganisha na wakati wa uhuru.” amesema Rais Samia wakati akisisitiza ongezeko la upatikanaji wa huduma za jamii.
Katika swala la Elimu na taaluma Rais Samia amesema kwa sasa Tanzania ina jumla ya vyuo vikuu 30 na vishiriki 17 wakati huo kilikua kimoja ikiwa shule za msingi ni 1746, huku idadi ya madaktari kwa uwiano ni daktari mmoja kwa wagonjwa elfu20 huku kukiwa na huduma nyingi za kibobezi ambazo nyingi hapo nyuma hazikutolewa.
Pamoja na hayo Rais Samia amesema katika kujenga heshima ya nchi kimataifa Tanzania imeshiriki na kushirikishwa kikanda na kimataifa katika mikutano mbalimbali, pia balozi za tanzania zimeongeseka katika nchi mbalimbali.
“Tuna urafiki na nchi zote duniani na hakuna nchi ambayo tuna uadui au mifarakano nayo, tunafanya kazi na mchi zote na kuheshimu misimamo ya nchi nyingine huku tukilinda maslahi ya diplomasia ya nchi yetu”
Swala la kuimarisha demokrasia ya wananchi Rais Samia amesema Nchi imekua na mfumo wa vyama vingi na kila mwananchi ana uhuru wa kuchagua chama anachokitaka na kuchagua kiongozi anaemtaka kila baada ya miaka 5 ikiwa wabunge waliokuwepo wakati wa uhuru ni 80 na sasa ni wabunge 393 na wanawake ni 133.
“Tuna mifumo ya kuwawezesha wananchi kutoa maoni bila bugudha, uhuru wa vyombo vya habari, huku mitndao ya kijamii ikiwapa watu uhuru wa kujieleza na kuhoji” Amesema Rais Samia
Katika kumalizia hotuba yake Rais Samia amewataka wananchi kufahamu kuwa hali na hadhi nchi iliyonayo kwa miaka 60 ndio muhimu kwa sasa na wito ni kudumisha amani mshikamano umoja na kutunza mazingira na kuyalinda kwa wivu mkubwa ili kurithisha vizazi vijavyo.
Rais Samia Suluhu Hassan amemalizia hotuba yake kwa kusema kuwa dira ya maendeleo ya mwaka 2025 ni kuangalia kukua kwa uchumi na dira ijayo itaelekeza kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla kwa sekta kama kilimo na ufugaji kwa maendeleo ya viwanda.