Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Bodi ya Ushauri ya Kituo cha Dunia cha Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi – GCA.
Taarifa ya uteuzi huo, iwasilishwa na Mwenyekiti wa Bodi ya GCA na Katibu Mkuu Mstaafu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, alipokutana na Rais pembezoni mwa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika Nairobi, Kenya.
Heshima hiyo, ni utambuzi wa uongozi mahiri wa Rais Samia katika jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi Afrika na duniani kote ambapo Tanzania ni kinara kwenye utekelezaji wa miradi mbalimbali barani Afrika.
Wajumbe wengine wa Bodi hiyo ni Rais wa Jamhuri ya Senegal, Macky Sall, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat, Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika – AfDB, Akinumwi Adesina na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Fedha wa Kimataifa – IMF, Kristalina Georgieva.
GCA ni taasisi kubwa duniani inayosimamia masuala ya uhimilivu wa mabadiliko ya tabianchi, ambapo hadi sasa imeweza kufanikisha upatikanaji zaidi ya Dola za Marekani bilioni 50, Tanzania ikiwa ni miongoni mwa nchi za kwanza zitakazonufaika na fedha hizo katika kipindi cha miaka mitatu ijayo.