Rais Samia Suluhu Hassan amewataka watanzania kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa, huku wakifuata mila, desturi na taratibu za nchi ambazo zinampa nafasi kila mwananchi kufanya kazi kwa uhuru na kwa kuhcagua kazi anayoitaka ili kuinynanyua nchi kimaendeleo.
Rais Samia amesema hayo akiwa katika mahojiano maalumu na Televisheni ya Taifa TBC Ikulu Chamwino, katika kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ambapo leo anatimiza miaka 62 ya maisha yake.
“Nina Ujumbe mmoja tu kwa watanzania na kila siku nawaambia, Duniani kuna nchi moja tu inayoitwa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na ndani ya hiyo nchi kuna watanzania ambao ni sisi lakini Mungu ametupanga kwa mamlaka mbalimbali, wito wangu ni mmoja tu, ‘Tufanye kazi kwa bidii’ kwa sababu tutakaojenga hii nchi ni sisi watanzania na tutakaoibomoa hii nchi ni sisi watanzania,” alisema Rais Samia.
Pia amewataka wasaidizi wake kuendelea kufanya maamuzi yao katika kutatua mahitaji ya wananchi na kumpunguzia yeye majukumu.
“Mimi katika majukumu yangu najitahidi mafaili yasikae kwangu, yakakae kwa wenzangu…kazi ni nyingi lakini ukiweza kuwatumia wasaidizi unapunguza kazi nyingi. Wao sijui kama ni kwa uoga au ni nini wanaleta maamuzi juu, lakini sisi hata katika mafunzo yao juzi tumewaambia ‘wasideligate maaumzi upward, ila wa deligate downwards’, wasaidizi wangu wanajua majukumu yao wananisaidia sana kuppunguza kazi,” Rais Samia.
Rais Samia pia katika mahojiano hayo ameweza kuzungumzia historia ya maisha yake ambapo amesema kwa mara ya kwanza alipata ajira akiwa na umri wa miaka 17.
Aidha Rais Samia pia ameweka wazi kuwa katika maisha yake jambo la kushtua zaidi ni swala la kumpoteza Rais wa Jamhuri ya Muungano hayati Magufuli na baada ya hapi ikalazimu yeye achukue nafasi hiyo.
Leo Januari 27, 2022, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassana ametimiza miaka 62 na katika wadhifa wa urais akieleka kutimiza mwaka mmoja.