Rais Samia Suluhu Hassan amesema wakati wa uzinduzi wa filamu ya Tanzania The Royal Tour jijini Dar es Salaam Mei 8 mwaka huu watawataja watu/taasisi zote zilizochangia fedha iliyotumika kutayarisha filamu hiyo inayoangazia fursa za utalii na uwekezaji nchini.
Rais Samia amesema hayo wakati wa mahojiano maalumu na yaliyofanywa na Azam TV, akisema katika uzinduzi wa Arusha waliwashukuru watu hao kwa ujumla, lakini Dar es Salaam watamtaja mmoja mmoja.
“Zile bilioni 7 sikuchukua serikalini, nilichangisha kwa wafanyabiashara ambapo watafaidika na yatakayotokana na ile filamu… Tutakapokuwa Dar es Salaam tutamtaja kila mmoja aliyechangia,” amesema.
Rais Samia amesema kiwango hicho cha fedha kinaweza kuonekana ni kikubwa, lakini kuzingatia ubora wa filamu hiyo yenye viwango vya Hollywood, na matokeo yake itakayoleta kwenye utalii, biashara na uwekezaji, yatakuwa ni makubwa huku akisisitiza kwamba anajua alichokifanya.
Aidha ameelezea rekodi za ulimwengu kwenye viwango vya rushwa ambapoTanzania bado imesisimama pazuri kwa kuwa hiyo siyo jitihada ya mwaka mmoja bali ni jitihada za miaka yote iliyofanywa na serikali.
”Mambo ni yale yale mimi sikuingia na yangu mimi nilikuwa makamu wa rais wa awamu ya tano ndiyo nilianza naye mwenzangu alivyoitwa na mungu, basi kazi yangu mimi ni kuendeleza yale aliyoyaacha, na katika kuendeleza kuna mambo kadhaa, kuna kurekebisha kuna kuweka vyema kuna kuongeza kuna kupunguza lakini mambo ni yale yale bado kazi tuliyoianza kule nyuma inaendelea vizuri kwenye madawa ya kulevya na kwenye rushwa pia.”