Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein amewataka wadau wa sekta binafsi nchini, kuweka mkazo katika utoaji wa huduma bora ili ziweze kukidhi viwango na ubora, kulingana na malengo na matarajio ya wananchi.
Dkt. Shein amesema hayo leo katika ukumbi wa Sheikh Idrissa Abdulwakil Kikwajuni Mjini hapa, alipofungua Jukwaa la Biashara la tisa (9) Zanzibar.
Jukwaa hilo ambalo limewashirikisha viongozi wa serikali na wadau mbali mbali wa sekta binafsi, limeambatana na kaulimbiu isemayo, “Ushirikiano baina ya sekta ya umma na Sekta binafsi katika kukuza Ajira kwa Vijana”
Akizungumza katika jukwaa hilo, Dkt. Shein alisema kumekuwepo na malalamiko kutoka miongoni mwa wananchi kuwa baadhi ya sekta binafsi zimekuwa zikiendesha shughuli za utoaji wa huduma,zisizokidhi mahitaji halisi pamoja na malengo ya taifa ya muda mfupi na mrefu.
Amesema kwa kiwango kikubwa malalamiko hayo yamekuwa yakielekezwa katika sekta za Afya na elimu, hivyo ametaka juhudi zifanyike kwa kuweka mkazo katika uimarishaji wa huduma bora.
Aidha, aliwataka wadau wa sekta hizo kuliangalia kwa kina suala la kuwajengea uwezo wafanyakazi wao, akibainisha kutokuwepo msukumo wa kutosha katika kuwasomesha wataalamu wa sekta hizo na badala yake kutegemea zaidi wataalamu waliosomeshwa na serikali.
“Hatua ya sekta binafsi kuajiri wataalamu walio na majukumu muhimu serikalini, kunaathiri utoaji wa huduma katika maeneo wanayoyatumikia, lazima muwe tayari kugharamika kwa ajili ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wenu”, amesema.
Amesema sio jambo jema kwa maendeleo ya taifa kwa kuwa na wataalamu wengi wasiopenda kufanyakazi katika sekta binafsi, kwa sababu ya ugumu wa kujiendel;eza.“Natowa wito kwa waajiri katika sekta binafsi kuwa na mipango imara ya kuwaendeleza wafanyakazi wenu’, amesisitiza.
Dkt. Shein akazipongeza sekta binafsi kwa kushirikiana na Serikali katika kuimarisha maslahi ya wafanyakazi, hususan kwa hatua yao ya kuitikia wito wa Serikali wa kupandisha mishahara ya kima cha chini kuambatana na miongozo iliyotolewa.
Aidha, amewataka waajiri wa sekta binafsi kuhakikisha wanafikisha michango ya wafanyakazi wao katika mfuko wa Hifadhhi ya jamii (ZSSF), ili kuwajengea wafanyakazi mustakbali mwema wa maisha yao na utulivu kazini.
Ameeleza kuwa sekta binafsi ina mchango mkubwa katika kufanikisha azma ya serikali ya kuwa na uchumi wa kati kwa kutumia fursa kadhaa ambazo bado hazijafikiwa.
Amezitaja baadhi ya fursa hizo kuwa ni pamoja na ile ya uvuvi wa bahari kuu, uendelezaji wa shughulli za kilimo na ufugaji kwa njia za kisasa pamoja uwekezaji katika sekta za nishati na viwanda.
“Tuwe na ujasiri wa kuwekeza katika sekta mpya ili kuepuka ushindani usio na lazima, bado hatujaanzisha miradi mipya kwa njia ya ubia kama wafanyavyo wenzetu katika nchi mbalimbali duniani’, alisema.
Amesema kuimarika kwa sekta binafsi kutapanua wigo wa soko la ajira na kuwapatia vijana kazi za staha kupitia sekta mbali mbali na hivyo kupata uwezo wa kuendesha maisha yao na pia kuongeza pato kwa Taifa.
Aidha, amepongeza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa za kuimarisha ushirikiano kati Serikali na sekta binafsi, kwa amslahi ya Taifa na wananachi wake.
“Ushahidi mzuri wa jambo hili ni ufanisi wa kupigiwa mfano ulioonekana katika maonyesho ya Utalii Zanzibar yaliofanyika hivi karibuni, tumeweza kuitangaza nchi kwa mafanikio makubwa’, alisema.
Kuhusiana na uimarishaji wa Mazingira ya Biashara, Dkt. Shein alisema Serikali imeanzisha sheria namba 10 ya mwaka 2017 kwa lengo la kuhakikisha kunakuwepo utaratibu bora na madhubuti katika uendeshaji wa biashara nchini.
Amesema Wafanyabiashara na wawekezaji hupenda kuwekeza katika nchi ambazo zimeweka mazingira mazuri ya kufanyia biashara, hivyo akaomba kuitumia mikutano na majukwaa kujadili namna bora ya kuimarisha na kurahisisha maendeleo katika sekta ya biashara.
“Utoaji wa huduma unaotegemea vitendo vya rushwa na uenyeji huzorotesha kasi ya biashara na uwekezaji, endelezeni shughuli zenu kwa kuzingatia mabadiliko ya teknolojia na mahitaji halisi ya wananchi’, amesema.
Mapema, Waziri wa Biashara na Viwanda, Balozi Amina Salum Ali alisema uanzishaji wa mabaraza ya Vijana utaongeza kasi ya kuzitafutia ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili vijana, hususan ya ukosefu wa ajira.
Amesema jukwaa hilo litajadili na kupata majibu ya mazingira bora yanayopaswa kuwepo ili kuleta maendeleo ya kibiashara sambamba na kukuza uchumi wa taifa.
Aidha, amesema ukosefu wa bajeti na chombo cha kuuunganisha sekta hizo mbili ni miongoni mwa changamoto zinazokwaza kupatikana kwa ufanisi.
Naye, Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyabiashara, wenye viwanda na wakulima, Taufiq Salim Turky akitoa salamu kutoka jumuiya hiyo kwa niaba ya sekta binafsi, alisema chini ya Uongozi wa Dk. Shein sekta ya utalii imepata mafanikio makubwa hususan katika suala la ujio wa watalii
nchini.
Amesema katika kipindi cha miaka minane ya Uongozi wake, ujio wa watalii umeongezeka kutoka ule wa watalii 150,000 uliodumu kwa takriban miaka 20 na kufIkia zaidi ya watalii 350,000 hivi sasa, huku kukiwa na matumaini makubwa ya kuongezeka kiwango hicho hadi kufikia 500,000 ifikapo mwaka 2020.
Amesema Rais Dkt. Shein amerejesha uelewa uliokosekana kwa kipindi kirefu, kuwa Serikali na sekta binafsi zina malengo ya aina moja.
Katika jukwa hilo, mada mbali mbali ziliwasilishwa na kujadiliwa.