Rais wa Algeria, Abdul Aziz Bouteflika ametangaza kuwa atajiuzulu nafasi hiyo ya juu ya uongozi, Aprili 28 mwaka huu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la taifa hilo, rais huyo ameeleza kuwa ataachia madaraka ili kutoa nafasi ya vyombo vingine vya nchi hiyo kuendelea na mchakato wa maandalizi ya uchaguzi katika kipindi cha mpito.
Awali, Rais huyo mwenye umri wa miaka 82 alitangaza kuwa atagombea tena urais ili kujiongezea muda wa utawala wake wa miaka 20, hadi pale maandamano makubwa ya kumpinga yalipoanza Februari mwaka huu.
Waandamanaji walianza harakati za kumtaka kuachia madaraka haraka. Hata alipobadili uamuzi wake kuwa hatagombea, waandamaji walimtaka kuachia madaraka kabla ya kipindi hicho ili asiingilie mchakato wa uchaguzi.
Jeshi la nchi hiyo kupitia kwa Mkuu wa Majeshi, limemtaka rais huyo kutangazwa kuwa hawezi tena kuendelea kuliongoza taifa hilo. Lilitoa wito kwa bunge la nchi hiyo kutafuta namna bora ya kisheria ambayo itawezesha kuondoka kuondolewa kwa rais huyo madarakani.
Rais Bouteflika amekuwa akionekana kwa nadra kwa umma, hasa baada ya kupatwa na kiharusi mwaka 2013.