Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 55, kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na Serikali ya nchi hiyo.
Serikali imetumia mtandao wa Twitter kuitaarifu dunia kuhusu kifo cha Nkurunzinza, ikieleza kuwa alifariki jana, Juni 8, 2020 baada ya kupata shambulio la moyo/mshtuko wa moyo.
Ujumbe huo katika ukurasa wa Twitter umesema, “Serikali ya Jamhuri ya watu wa Burundi inatangaza kwa masikitiko makubwa kifo kisichotarajiwa cha mheshimiwa Pierre Nkurunziza, Rais wa Jamhuri ya Burundi, kufuatia ugonjwa wa moyo Juni 8, mwaka 2020.”
Serikali ya Burundi imetangaza siku saba za maombolezo na ametuma salamu za ramirambi kwa familia.
Aidha, serikali imeeleza kuwa baada ya hali yake kuwa mbaya alilazwa katika hospitali ya Karusi, lakini juhudi za kuokoa maisha yake hazikufanikwia.
Alikuwa madarakani tangu mwaka 2005, na mwaka huu alipata mrithi wa kiti cha urais baada ya Evariste Ndayishimiye kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanyika Mei 20 mwaka huu.
Ndayishimiye ni Rais Mteule wa Burundi na anasubiri kuapishwa ili achukue rasmi nafasi ya urais.
Nkurunziza alikuwa Mwenyekiti wa chama tawala cha CNDD-FDD.
Matumaini: ujenzi meli za New MV Victoria na MV Mwanza umefikia 98%
Walichosema waliompiga Mbowe, Kamanda Muroto, Naibu Spika, Mnyika wazungumza