Kamati ya nidhamu ya Shirikisho la Soka la duniani FIFA, imemuadhibu kwa kumfungia miaka mitano Rais wa Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF Ahmad Ahmad, baada ya bodi ya uendeshaji ya shirikisho hilo kuridhia.

Taarifa kutoka FIFA zinaeleza kuwa, kiongozi huyo amefungiwa kujihusisha na mchezo wa soka na shughuli zote zinazohusiana na mchezo huo pendwa duniani, kufuatia kubainika alikua na matumizi mabaya na ufujaji wa fedha za CAF akiwa madarakani.

Kamati ya nidhamu ya FIFA iliyosimamia kesi ya kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 60, imejiridhisha ukweli wa tuhuma zilizomkabili, na kufikia muafaka wa kumpa adhabu hiyo, ambayo haijawahi kutokea kwa kiongozi wa ngazi ya juu (Rais) wa CAF.

Taarifa hiyo imeendelea kubainisha kuwa, Ahmad amekuwa kwenye uvunjifu wa taratibu zilizowekwa na kwenye masuala ya matumizi ya fedha kwa muda mrefu.

“Uchunguzi juu yake umefanywa kwa muda mrefu na ilianza baada ya kuingia madarakani 2017-2019 kuna mambo yalikuwa hayapo sawa kwenye masuala ya mipango na matumizi.” Imeeleza taarifa hiyo.

Ahmad aliingia madarakani mwaka 2017 kwa kushinda uchaguzi dhidi ya aliyekua rais wa FIFA kwa kipindi kirefu Issa Hayatou, na mara kadhaa alikabiliana na changamoto kadhaa, zikiwemo za ufujaji wa fedha ambazo zimemuangusha.

Jicho la UN laitazama Ethiopia
Azam FC yaitangazia njaa Young Africans