Rais wa Iran, Hassan Rouhani amekosoa vikali hatua ya Marekani kuweka vikwazo vipya dhidi ya kiongozi mkuu wa kidini nchini humo, Ali Khamenei. Amedai kuwa hatua hiyo ni ya kijinga na inaonesha Ikulu ya Marekani ina utindio wa ubongo.
Akizungumza leo kupitia Televisheni ya Taifa, Rais huyo wa Iran amesema kuwa vikwazo hivyo dhidi ya Khamenei vitashindwa kwa sababu hana mali nje ya nchi.
“Vitendo vya Ikulu ya Marekani vinaonesha kuwa ina utindio wa ubongo,” alisema Rouhani na kuongeza kuwa ukimya wao wa kimkakati usichukuliwe kama ishara ya uoga.
Rais wa Marekani, Donald Trump, jana alitangaza vikwazo vipya dhidi ya Khamenei ambaye anadaiwa kuwa muwezeshaji mkuu wa kifedha kwa Jeshi la Mapinduzi la nchi hiyo.
Vikwazo hivyo pia vimewalenga baadhi ya viongozi waandamizi wa Iran ikiwa ni pamoja na mawaziri.
Naye Trump ametumia akaunti yake ya Twitter kumjibu Rais wa Iran akidai kuwa hajui anachokizungumza.
Rais Trumnp alijigamba kuwa nchi yake ndiyo nchi yenye jeshi imara zaidi duniani na kwamba watatoa adhabu kali kwa Iran endapo watafanya jambo lolote linaloashiria uchokozi wa kijeshi.
“Kitu chochote kitakachofanywa na Iran juu ya Mmarekani yeyote kitajibiwa na nguvu kubwa, na kwa wakati mwingine adhabu inaweza kuwa ni kutokomeza baadhi ya sehemu,” Trump aliongeza.
Taharuki kati ya nchi hizo inatokana hasa na Iran kuidungua ndege ya Marekani isiyo na rubani. Iran ilikiri kuitungua ndege hiyo na kueleza kuwa iliingia kwenye anga lake. Marekani imeendelea kukanusha ikieleza kuwa ilikuwa katika anga la kimataifa.
Awali, Trump alitangaza kufuta mpango wa nyuklia wa mwaka 2015 ulioasisiwa na aliyekuwa Rais wakati huo, Barack Obama. Iran nayo ikatangaza kuendelea kutengeneza nyuklia, ikiilaumu Marekani kwa kuvunja makubaliano yaliyokuwa kwenye mkataba.