Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera amewapiga kalamu nyekundu mawaziri wote katika baraza lake kuhusiana na madai ya ufisadi.
Katiba hotuba yake kwa taifa siku ya Jumatatu, Januari 24, Chakwera aliapa kukabiliana na aina zozote za uvunjaji wa sheria wa maafisa wa umma akisema majukumu yote ya mawaziri hao sasa yatasimamiwa na ofisi yake hadi atakapotangaza baraza jipya ya mawaziri.
“Nimevunja baraza langu lote la mawaziri mara moja, na majukumu yote ya baraza la mawaziri yatarejea ofisini kwangu hadi nitakapotangaza baraza la mawaziri lililoundwa upya baada ya siku mbili,” Chakwera alisema katika hotuba yake ya kitaifa.
Aliongeza kuwa baraza la mawaziri litakaloundwa upya litamtenga Waziri wa Ardhi Kezzie Msukwa, ambaye alikamatwa mwezi uliopita katika kesi ya rushwa ili aweze kujibu mashtaka.
Duru za kisiasa nchini humo zinzsema kuwa uamuzi huo wa kushangaza unafuatia mikutano kadhaa iliyofanywa wiki jana na makundi mawili yenye ushawishi mkubwa nchini humo.
Makundi hayo ni Baraza la Maaskofu la Malawi na Kamati ya Masuala ya Umma, ambayo inajumuisha vikundi vya makanisa ambavyo vinafanya kazi kama walinzi wa serikali.
Makundi yote mawili yalielezea wasiwasi wake kwa rais kutochukuwa hatua katika kupambana na ufisadi. Chakwera alishinda uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, akiahidi kupambana na ufisadi katika nchi hiyo maskini kusini mwa Afrika.