Rais wa Mali, Ibrahim Boubacar Keita amejiuzulu saa chache baada ya jeshi la nchi hiyo kumzuia katika nyumba yake kufuatia maandamano ya wananchi yaliyodumu kwa miezi mitatu, wakidai kupinga vitendo vya rushwa na kutokuwa na uhakika wa usalama.
Taarifa za kujiuzulu kwa Keita zimeibua shangwe kwa waandamanaji, huku jeshi lililomzuia likitangaza kuwa litashika madaraka na kuitisha uchaguzi katika muda unaowezekana.
Mwanasiasa huyo alitangaza uamuzi wake wa kujiuzulu majira ya usiku wa kuamkia leo, alipokuwa akilihutubia taifa hilo kupitia Televisheni ya Taifa. Keita mwenye umri wa miaka 75 amechukua uamuzi huo huku akiwa na kipindi cha miaka mitatu iliyosalia kumaliza muhula wake wa urais.
Mwakyembe: Morrison ametupotezea muda
Sambamba na uongozi huo, ametangaza kuvunja Baraza la Mawaziri na kuiweka rasmi kuwa Serikali yake imefika ukomo.
“Kama leo, kuna chembechembe za wanajeshi wetu wanaotaka awamu hii iishe kwa kuingilia kati, mimi kweli nina chaguo?,” Keita alisema akiwa kwenye ngome ya kijeshi katika mji wa Kati, nje kidogo ya Mji Mkuu Bamako.
Keita aliongozana na Waziri Mkuu, Boubou Cisse ambaye kwa pamoja walikuwa wanashikiliwa na jeshi la nchi hiyo.
“Sihitaji kuona damu inamwagika ili mimi nibaki madarakani, nimeamua kujiuzulu na kuachia ofisi,” aliongeza Keita.
Saa chache baadaye, wanajeshi ambao walishiriki mapinduzi hayo, wanaojiita ‘National Committee for the Salvation of the People’, lilitokea kwenye televisheni ya taifa wakiahidi kuituliza nchi hiyo.
“Hatuna lengo la kushika madaraka, lakini tuna nia ya kuhakikisha nchi inaimalika na utulivu unarejea,” alisema Ismail Wague, Naibu kiongozi wa jeshi hilo.