Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ameitaka Benki Kuu kuhakikisha haitoi fedha za kigeni kwa ajili ya ununuzi wa vyakula kutoka nje ya nchi kwa lengo la kuinua sekta ya kilimo nchini humo.
Rais Buhari ameeleza kuwa fedha za kigeni zilizoko Benki Kuu zinapaswa kutunzwa na kutumika pale ambapo kuna hitaji la msingi linaloweza kuinua uchumi wa nchi na sio kuhamasisha utegemezi wa vyakula kutoka nje.
“Usitoe hata senti moja kwa mtu yeyote kwa ajili ya kuingiza chakula nchini,” msemaji wa Rais Buhari, Garba Shehu amemkariri kiongozi huyo kupitia mtandao wa Twitter.
Nigeria ni taifa lenye nguvu zaidi ya kiuchumi barani Afrika ikiwa na watu takribani milioni 200, lakini imekuwa ikitegemea vyakula kutoka nje ya nchi.
Rais Buhari ambaye alishinda uchaguzi kwa awamu ya pili mapema mwaka huu, aliwaahidi wananchi wake kuwa atahakikisha uchumi wa nchi unakuwa pia kupitia sekta ya kilimo.
Uchumi wa Nigeria unategemea zaidi sekta ya viwanda na uzalishaji wa mafuta ambao umeifanya kuwa taifa linaloongoza kwa uchumi Afrika.